Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UM yaungana kuadhimisha siku ya chakula duniani

Mashirika ya UM yaungana kuadhimisha siku ya chakula duniani

Katika kuadhimisha siku hii ya chakula duniani, mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa pia yametaja umuhimu wa mashirika katika kuulisha ulimwengu. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ajira Duniani, ILO, Guy Ryder, amesema mashirika haya yana mchango muhimu kuhakikisha haki ya kuwa na chakula inafurahiwa na wote, wakati huu ambapo watu milioni 870 wana upungufu wa lishe.

Naye rais wa hazina ya kimataifa kuhusu maendeleo ya kilimo (IFAD) Kanayo Nwanze, amesema hazina hiyo hushirikiana kwa karibu na mashirika ya wakulima kote duniani, kwani mashirika haya huwasaidia wakulima wadogo katika kudhibiti uzalishaji wao vyema, na katika kuongeza nafasi na rasilmali zao.

Akizungumza kuihusu siku hii, Mkurugenzi Mkuu wa WFP, Ertharin Cousin amesema kuna haja ya kuweka mfumo wa kuwasaidia watu ambao hawajiwezi kabisa, hasa wanawake na watoto, kwa kuweka viwango wastani vya ulinzi wa kijamii. Amesema hiyo ndio njia pekee ya kuwainua kutoka lindi la umaskini na njaa.