Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumaini ya Israeli na Palestina kumaliza mgogoro kwa kuwa mataifa mawili yanafifia: Feltman

Matumaini ya Israeli na Palestina kumaliza mgogoro kwa kuwa mataifa mawili yanafifia: Feltman

Uwezekano wa kuwa na taifa la Palestina na Israeli kama suluhisho la mgogoro kati yao unaonekana kupungua. Hiyo ni kauli ya afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman aliyoitoa mbele ya kikao cha Baraza la Usalama la Umoja huo jijini New York, Marekani hii leo.

Feltman ambaye ni mkuu wa masuala ya siasa ndani ya Umoja wa Mataifa amesema pande zote mbili bado zinaendelea kushikilia kile alichokiita ni msimamo wa kifikra zaidi wa majadiliano ya amani.

Hata hivyo amesema msimamo huo hautafsiriki katika hatua ambazo zinaweza kurejesha upya majadiliano kwenye masuala ya kimsingi, huku akionya kuwa ghasia na vyanzo vingine vya hali ya wasiwasi vimesababisha kushindwa kuondokana na mkwamo wa kisiasa.

"Tuna matumaini kuwa maendeleo ya sasa yanaweza kushughulikiwa katika hali ambayo italeta mafanikio na tunakumbusha kila mmoja kuwa suluhu kupitia majadiliano ya kuwa na mataifa mawili, ambayo viongozi wa pande zote wanatambua inapaswa kubakia kipaumbele cha ju. Tuna hofu , hata hivyo kuwa fursa ya suluhisho la aina hiyo inaweza kufungwa.”