Syria, sitisheni mapigano wakati wa Sikukuu ya Eid El Haji:Brahimi

15 Oktoba 2012

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi ameiomba Iran isaidie kufanikishwa kwa usitishaji wa mapigano nchini Syria wakati wa sikukuu ya Eid El Haji, wiki ijayo, siku ambayo amesema ni moja ya tukufu zaidi miongoni mwa waumini wa dini ya kiislamu duniani kote.

Bwana Brahimi ametoa rai hiyo baada ya kumaliza ziara yake nchini Iran ambako alikuwa na mazungumzo na Rais Mahmoud Ahmadinejad, Waziri wa Mambo ya Nje Ali Akbar Salehi na Katibu uwa Baraza Kuu la usalama wa kitaifa nchini humo Saeed Jalili.

Katika mazungumzo hayo, mjumbe huyo amesema mgogoro wa Syria unazidi kuongezeka siku hadi siku na kusisitiza umuhimu wa kuacha vitendo vya umwagaji damu.

Tayari Bwana Brahimi amewasili Baghdad, Iraq kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo akiwemo Waziri Mku Nouri Al Maliki kuhusiana na mgogoro huo wa Syria ikiwa ni sehemu ya awamu ya pili ya ziara yake kwenye eneo hilo kujaribu kuharakisha jitihada za kumaliza mgogoro huo ambapo tayari ameonana na viongozi wa Saudi Arabia na Uturuki.

Katika awamu ya kwanza ya ziara ya aina hiyo alikutana na viongozi wa Umoja wa nchi za kiarabu nchini Misri, iliyofuatiwa na mazungumzo na Rais Bashar Al Assad wa Syria lakini hadi sasa hakuna maendeleo ya dhati yaliyofikiwa kumaliza mgogoro wa Syria.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud