Brahimi na Mfalme Abdallah wa Saudia wajadili mzozo wa Syria

12 Oktoba 2012

Mgogoro wa Syria umekuwa ajenda ya mazungumzo kati ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi na msimamizi wa misikiti miwili mitakatifu nchini Saudi Arabia, Mfalme Abdallah Bin Abdelaziz al Saud.

Katika mazungumzo yao huko Jeddah, wawili hao wamekubaliana kuwa hali ya usalama nchini Syria inazorota siku hadi siku na kusababisha madhila yalojificha kwa raia wa nchi hiyo.

Hivyo basi wamesema kuna umuhimu mkubwa wa kusitisha vitendo vya umwagaji damu na kuwapatia misaada ya kibinadamu zaidi ya raia Milioni Mbili na Nusu walioathiriwa na mzozo huo nchini humo pamoja na wakimbizi 348,000 walioandikishwa nchi jirani.

Brahimi ambaye ni mmoja wa wajumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Syria, ametathmini mazungumzo kati yake na serikali ya Syria na waasi na kusisitiza imani yake kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kijeshi bali kwa njia ya kisiasa itakayokidhi matakwa ya raia wa nchi hiyo.

Tayari Brahimi ameshakuwa na mazungumzo ya kina na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, mwanamfalme Abdelaziz Bin Abdallah kuhusu mgogoro wa Syria.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud