Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UM yaadhimisha siku ya mtoto wa kike kwa upinga ndoa za wasichana wenye umri mdogo

Mashirika ya UM yaadhimisha siku ya mtoto wa kike kwa upinga ndoa za wasichana wenye umri mdogo

Nayo mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaadhimisha siku hii kwa kulimulikia suala la ndoa za wasichana wenye umri mdogo, ambazo hukiuka haki za binadamu na kuathiri vibaya mno nyanja zote za maisha ya mtoto wa kike. Shirika la Kuhudumia Watoto la UNICEF, limesema siku hii inaonyesha haja ya kuweka mahitaji ya mtoto wa kike kwenye nguzo ya kati ya maendeleo.

Afisa wa kitengo cha jinsia na haki cha shirika hilo, Anju Malhotra, amesema, Umoja wa Mataifa na wadau wengine wanaungana kwenye siku hii kuonyesha hatua zilizopigwa, na changamoto zinazoendelea kuwepo.

Naye Mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa cha UN Women, Michelle Bachelet, amesema wasichana wana haki ambazo zinastahili kuheshimiwa. Ameongeza kuwa iwapo wasichana wataendelea kukumbwa na dhuluma na ubaguzi, kupozwa bila hiari, kunyimwa sauti zao na nafasi ya kuchagua, kunyimwa matumaini na ndoto zao, pamoja na kudhihirisha uwezo wao, UN Women itasimama nao

Wasichana wanataka haki sawa, nafasi sawa, na kuhusishwa katika masuala yote.Sote tunazaliwa tukiwa sawa, lakini wasichana wengi sana wanakumbwa na ukatili na dhuluma za ngono. Wasichana milioni 32 hawapo katika shule za msingi, na wengi hupozwa wakiwa wangali wadogo sana. Wasichana kote duniani wanataka sauti zao zisikike, na wanataka haki zao ziendelezwe na kulindwa. Utafiti unaonyesha kuwa kuwekeza katika wasichana, ni njia bora zaidi ya kupunguza umaskini, kuboresha viwango vya afya na elimu, na kuendeleza usawa. Tunahitaji kuiga kutoka kwa wasichana, na kuunga mkono ujasiri na ubunifu wao. Wasichana wanaponyimwa nafasi ya kudhihirisha uwezo wao, ni hasara kwa wote.