Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu pekee kumuepusha mtoto wa kike na ndoa za umri mdogo: Ban

Elimu pekee kumuepusha mtoto wa kike na ndoa za umri mdogo: Ban

Ikiwa leo ni maadhimisho ya kwanza ya kimataifa ya siku ya mtoto wa kike, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametaka serikali duniani kuchukua hatua kuwaepusha watoto wa kike na ndoa za umri mdogo.

Katika taarifa yake, amesema ndoa za watoto hufanyika zaidi vijijini kwenye maskini na iwapo hali ya sasa itaendelea idadi ya wasichana watakaoolewa kabla ya kufikisha miaka 18 itaongezeka na kufikia Milioni 150 muongo ujao, kitendo ambacho kinahatarisha afya zao na hata kupoteza fursa za kujiendeleza kielim.

Ban amesema elimu pekee ndio mkakati bora wa kuwazuia watoto wa kike kuolewa katika umri mdogo na ametaka serikali, sekta binafsi, taasisi za kiraia na za kidini kuwekeza katika kuendeleza haki za mtoto wa kike kupitia mikataba ya kimataifa ikiwemo ule wa haki za mtoto na ule wa kuzuia vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Ujumbe wa siku ya mtoto wa kike duniani hii leo ni "Maisha yangu, haki yangu, komesha ndoa kwa mtoto".