Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani shambulizi la kundi la Taliban dhidi ya wasichana wa shule

UM walaani shambulizi la kundi la Taliban dhidi ya wasichana wa shule

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na vita vya silaha, Leila Zerrougui, amelaani vikali shambulizi lililotekelezwa na watu wenye silaha kutoka kundi la Taliban dhidi ya wasichana wa shule kwenye bonde la Swat, kaskazini magharibi mwa Islamabad, nchini Pakistan.

Msemaji wa kundi la Tehrik-i-Taliban Pakistan (TTP) amedai kuwa ni wao walitekeleza shambulizi hilo, ambao lilimjeruhi vibaya msichana mwenye umri wa miaka 14, ambaye ni maarufu kwa kupinga kufungwa kwa shule za wasichana na kundi hilo katika bonde la Swat. Msichana huyo alijeruhiwa pamoja na wasihana wengine wawili wa shule katika basi la shule, karibu na shule yao.

Malala Yousufzai alijulikana kama mwanaharakati mwenye umri mdogo, na sauti thabiti kuhusu elimu ya watoto wasichana, na alipokea tuzo ya ngazi ya juu zaidi kutoka kwa serikali ya Pakistan kwa raia wa kawaida, mnamo mwaka 2011. Msichana huyo bado anapokea vitisho kutoka kwa kundi  la TTP.

Bi Zerrougui amewatakia wasichana hao nafuu haraka, na kutuma ujumbe wa kutia moyo kwa familia na jamaa za waathiriwa. Amesema kundi la TTP ni lazima liheshimu haki ya watoto wote kupata elimu, wakiwemo wasichana.