Wakuu wa vikosi vya amani wakutana Dakar kujadilia amani ya Afrika Magharibi

9 Oktoba 2012

Wakuu wa vitendo vya operesheni ya amani vya Umoja wa Mataifa ambao wamekutana huko Dakar Senegal kwa ajili ya kujadilia hali ya mambo katika eneo la afrika magharibi wamehimiza haja ya kuongeza mashirikiano kwa ajili ya kutanzua mkwamo unaolikumba eneo hilo.

Wakuu hao walikutana kwa shabaha ya kupeana taarifa za namna ya kuboresha hali ya usalama na kudumisha amani kwenye eneo hilo ambalo linaandamwa na mikwamo ya kisiasa iliyosababisha kujitokeza vitendo vya umwagikaji wa damu.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Afrika Magharibi Bwana Said Djinnit, ambaye ndiye aliyeendesha kikao hicho alihimiza haja ya kukaribisha mashirikiano ya kikanda kwa ajili ya kuzikabili changamoto za kiiusalama na akitolea mfano hali iliyojitokeza hivi karibuni nchini Ivory Coast ambako kuliibuka hali ya sintofahamu baina yake na jirani yake Liberia kuhusiana na mzozo wa mpakani.

Viongozi hao pia walijadilia mkwamo wa madaraka nchini Guine-Bissau ambako walizihimiza pande zinazohasimiani kuendelea kuyaunga mkono majadiliano ya upatanishi yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa.