Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Boti yazama ikielekea Mayotte, watu sita wafariki dunia

Boti yazama ikielekea Mayotte, watu sita wafariki dunia

Watu sita wamefariki dunia na wengine kumi bado hawajulikani waliko baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama mapema Jumatatu karibu na kisiwa cha Mayotte kilicho chini ya himaya ya Ufaransa.

Hii ni ajali ya pili ya aina hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja na inahusisha wakimbizi na wahamiaji haramu wanaotafuta maisha bora kwenye kisiwa cha Mayotte ili kukwepa umaskini, manyanyaso na vita katika nchi zao, na inafanya idadi ya watu waliokufa au kupotea karibu na kisiwa cha Mayotte kufikia 69 mwaka huu.

Habari zinasema kwa miongo kadhaa sasa watu wasio na nyaraka zinazotakiwa wamekuwa wakitumia boti za wazi maarufu kama KWASSA-KWASSA kwa ajili ya kusafiri kutoka visiwa vya Comoro hadi Mayotte.

Mwaka jana idadi ya watu waliokuwa wakitafuta hifadhi hko Mayotte ilikuwa Elfu Moja Mia Mbili, ikiwa ni ongezeko la asilimia 41 ikilinganishwa na mwaka 2010 na wanatoka Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Madagascar, Rwanda na Burundi.