Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na rais wa Ufaransa kujadili mizozo ya Syria na eneo la Sahel

Ban akutana na rais wa Ufaransa kujadili mizozo ya Syria na eneo la Sahel

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amekutana na Rais Francois Hollande wa Ufaransa mjini Paris na kujadili kuhusu mizozo inayoendelea nchini Syria na katika eneo la Sahel. Kuhusu mzozo wa Syria, Bwana Ban amerejelea wito wake wa kukomesha ghasia na kupatia silaha vikundi vinavyozozana, pamoja na kufanya maandalizi ya serikali ya mpito, yakiendeshwa na watu wa Syria.

Amesema kuenea kwa mzozo huo kwenye mpaka wa Syria na Uturuki na athari zake kwa Lebanon na nchi zingine jirani ni hatari, na umekuwa janga la kikanda ambalo linaathiri ulimwengu mzima.

Kuhusu hali katika eneo la Sahel, Bwana Ban amesema kuwa Umoja wa Mataifa unaandaa mkakati wa kina kuhusu masuala ya kimataifa kwenye eneo zima la Sahel, yakiwemo silaha, wakimbizi na ugaidi. Ameongeza kwamba amependekeza kuwa Baraza la Usalama limteue aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Romano Prodi, kama mjumbe maalum kwa eneo la Sahel.