Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Anwani za makazi ni muhimu kwa maendeleo: Profesa Tibaijuka

Anwani za makazi ni muhimu kwa maendeleo: Profesa Tibaijuka

Mkutano mkuu wa 25 wa Umoja wa posta duniani, UPU, umeanza leo uko Doha, Qatar ambapo balozi maalum wa UPU kuhusiana na anwani za makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema watu wasiokuwa na anwani wametengwa na wanashindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Akizungumza katika mjadala kwenye mkutano huo wa siku tano unaoangalia hatma ya posta,  Profesa Tibaijuka amesema uhaba wa mfumo sahihi wa anwani ya makazi  ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa wakazi masikini wa mijini kwa sababu unawaengua katika mifumo sahihi ya miji na wanashindwa kupata huduma muhimu kama nyumba, huduma za jamii na zile za kifedha.
Balozi huyo maalum wa UPU amekiri umuhimu wa posta katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na kusema kuwa hivi sasa dunia inaishi katika enzi za kuendeleza utawala bora, utawala wa kisheria na hivyo itakuwa vigumu nchi kuhakikisha kuna ukweli na uwazi katika chaguzi iwapo idadi kubwa ya wapiga kura hawajaandikishwa kwa sababu hawana anwani za makazi.