UNHCR yatoa mwongozo wa kuwalinda wanaume wanaobakwa

8 Oktoba 2012

Kwa mara ya kwanza Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetoa mwongozo utakaosaidia kuwatambua na kuwasaidia wanaume waliokumbwa na visa vya kubakwa au manyanyaso ya kingono katika mazingira ya migogoro na ukimbizi.

Mwongozo huo ulioandaliwa na kitengo cha usalama wa kimataifa cha UNHCR utatumiwa na wafanyakazi wa shirika hilo na wale wa msaada na umezinduliwa hivi karibuni mjini Geneva, Uswisi katika mjadala juu ya suala hilo ambalo ni nadra kutajwa.

Naibu Mkurugenzi wa kitengo hicho Louise Aubin amesema wametoa mwongozo huo kwa sababu ni muhimu kujifunza jinsi ya kutangamana na waathirika wa vitendo vya ubakaji na kuondoa vikwazo vyovyote vya kuripoti matukio hayo ili waathirika waweze kupata msaada bila kujali jinsi yao.

Mjadala huo ulioshirikisha wanaharakati wanawake na wanadiplomasia ambapo Profesa Sandesh Sivakumaran kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham nchini Uingereza amesema manyanyaso ya kingono na kijinsia dhidi ya wanaume na wavulana hutajwa kwa kifupi sana katika ripoti wakati ambapo suala la ubakaji siyo la jinsi moja pekee na kwamba inapaswa kutambuliwa kuwa ubakaji ni mateso na kubakwa ni kubakwa.

Hata hivyo mpaka sasa hakuna takwimu za kina kuhusu idadi ya wanaume waliokumbwa na vitendo hivyo

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud