Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aahidi ushirikiano zaidi baada ya miaka 20 ya makubaliano ya amani Msumbiji

Ban aahidi ushirikiano zaidi baada ya miaka 20 ya makubaliano ya amani Msumbiji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon ameipongeza Msumbiji kwa kusherehekea miaka 20 tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani ya mwaka 1992 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenye vilivyoibuka mara baada ya kupata uhuru mwaka 1975.

Msemaji wa Ban amemkariri Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akisisitiza kuwa ofisi yake itaendeleza ushirikiano na nchi hiyo wakati huu inapoimarisha demokrasia na kujitahidi kuleta utangamano wa kijamii, kuwaendeleza wanawake na kujiletea maendeleo endelevu.

Ban amekumbusha operesheni iliyofanywa na kilichokuwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Msumbiji, ONUMOZ kati ya mwaka 1992 na 1994, operesheni ambayo amesema ilisaidia kutekeleza makubaliano ya amani na kuweka msingi wa kudumu wa amani.

Msumbiji mara baada ya uhuru wake ilingia katika mapigano kati ya serikali na kikundi cha RENAMO ambapo mwaka 1992 pande hizo zilikubaliana kumaliza vita na kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.