Makazi kwa wakimbizi wa Syria nchini Lebanon bado ni tatizo: UNHCR

Makazi kwa wakimbizi wa Syria nchini Lebanon bado ni tatizo: UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema uhaba wa makazi utaendelea kuwa tatizo kubwa kwa sasa na baadaye kwa wakimbizi wa Syria nchini Lebanon.

Afisa wa UNHCR anayehusika na hifadhi ya wakimbizi hao Anna Leer akizungumza mjini Tripoli, Libya amesema yeye na watendaji wengine wamebaini kuwa wakimbizi hao wamesambaa maeneo mbali mbali nchini Lebanon na kwamba uwezo wa wenyeji kuendelea kuutoa hifadhi unapungua siku hadi siku na gharama ya kodi ya nyumba imepanda mara nne zaidi.

Hata hivyo UNHCR kwa kushirikiana na Norway na Denmark imeanza kuchukua hatua za msaada wakati huu msimu wa baridi kali unapokaribia. Mathalani makazi 27 ya pamoja yamefanyiwa ukarabati kwa msaada wa Norway huku UNHCR na Denmark kwa pamoja zikitengeneza nyumba 60 kwa gharama ya dola 2,500 kila moja kwa familia zilizoko Kaskazini mwa Lebanon zinazoishi kwenye mahema au makazi yasiyokamilika.

UNHCR pia inawasiliana na mamlaka husika kuona ni jinsi gani zinaweza kusaidia familia kupata makazi mbadala baada ya baadhi ya shule kwenye jimbo la Bekaa zilizotumika kuhifadhi wakimbizi wakati wa msimu wa joto, sasa kuhitajika kwa ajili ya masomo.

Katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu zaidi ya raia 70,000 wa Syria wamekimbilia Lebanon kutafuta hifadhi kutokana na mgogoro nchini mwao na idadi hiyo inaweza kuongezeka iwapo mgogoro nchini mwao utaendelea.