Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waziri Mkuu wa China atunukiwa tuzo ya juu ya UM kuhusu chakula

Waziri Mkuu wa China atunukiwa tuzo ya juu ya UM kuhusu chakula

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la chakula na Kilimo, FAO leo limemtunuku Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao leo tuzo ya juu ya Umoja huo kutokana na mchango wake wa kuongeza uzalishaji wa chakula na hivyo kusaidia kupunguza idadi ya watu mafukara duniani.

Akikabidhi tuzo hiyo mjini Beijing, China, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema kasi ya kupunguza idadi ya watu maskini duniani imeharakishwa na China ambayo kupitia jitihada za dhati za Waziri Mkuu Wen imesaidia kuwepo uhakika wa chakula na kupunguza umaskini miongoni mwa raia wake na duniani kwa ujumla.

Kwa upande wake Wen amesema bila mageuzi ya kisasa kwa sekta ya kilimo na vijiji nchini China uchumi wa Taifa hilo usingeendelea kwa kasi ya sasa akieleza kuwa nchi yake imekuwa na ongezeko la uzalishaji wa chakula kwa mwaka wa tisa mfululizo tangu mwaka 2003.

Kwa mujibu FAO China tayari imeanzisha mfuko wa dola Milioni 30 za kimarekani chini ya ushirikiano kati ya FAO na nchi zinazoendelea kwa ajili ya kusaidia kuboresha mbinu za kilimo katika nchi za Afrika, Asia, Caribbean na kusini mwa Pasifiki.