Baraza Kuu la UM lahitimisha mkutano wake wa kila mwaka

Baraza Kuu la UM lahitimisha mkutano wake wa kila mwaka

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesema mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu umedhihirisha tena umuhimu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya diplomasia, katika kuweka kanuni za kimataifa na katika kuleta pamoja nguvu za ushirikiano katika maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo, Bwana Eliasson amesema mikutano ilofanyika ya ngazi za juu na mingineyo imetoa msukumo wa kupiga hatua zaidi, hasa katika kukabiliana na suala sugu la hali ya eneo la Sahel. Hatua pia zimepigwa kuhusu suala la ugaidi wa nyuklia, kuunga mkono mabadiliko ya kisiasa katika nchi za Myanmar, Somalia na Yemen, pamoja na kuwezesha kusainiwa kwa mktaba wa kupunguza uhasama baina ya Sudan na Sudan Kusini

Mkutano huo wa 67 wa Baraza Kuu umehitimishwa Jumatatu jioni, baada ya hotuba kutoka kwa zaidi ya viongozi 190, wakiwemo marais na makamu wa rais, mawaziri na wajumbe wa kiplomasia. Akiufunga mkutano huo, rais wa Baraza Kuu Vuk Jeremic amesema kuwa mataifa yote wanachama yamechangia kwa njia muhimu suala la utatuzi wa mizozo kwa njia ya amani, ambayo ilikuwa mbiu mgambo ya kikao cha mwaka huu.