Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya ajira ni muhimu ili kujikwamua kiuchumi

Haki ya ajira ni muhimu ili kujikwamua kiuchumi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani, ILO Guy Ryder amesema viwango vya ajira vya kimataifa vinapaswa kuzingatiwa na kuendelezwa iwapo mataifa yanataka kujikwamua kiuchumi na kuondokana na ukosefu wa ajira wakati huu ambapo shirika hilo linakadiria kuwepo kwa zaidi ya vijana Milioni 75 duniani wasio na ajira.

Ryder ambaye amechukua wadhifa huo kutoka kwa Juan Somavia aliyemaliza muda wake wa kuongoza shirika hilo , amesema suala la kuongeza ajira lisiwe kisingizio cha kupuuza mazingira bora ya kazi na kwamba tatizo la uchumi duniani litamalizika iwapo vijana watapatiwa ajira.

Ushahidi unaonyesha iwapo kijana anakosa kazi kwa kipindi cha mwaka wa kwanza au wa pili wa kipindi cha kujiendeleza kiajira, hali hiyo inamuathiri maisha yake yote. Hana njia yoyote. Kwa hiyo tunapaswa kuchukua hatua haraka tena sasa kuwalenga vijana. Njia mojawapo ya kufanya ni kuangalia mipango ya wao kujipatia uzoefu au mafunzo zaidi iwapo wanakuwa hawana kazi wala hawaendi shule. Inaonekana ni gharama lakini inawezekana kwani tunakuwa tumewekeza. Hii ni mojawapo ya vipaumbele ambavyo ILO inabidi izingatie zaidi katika miezi ijayo kwa sababu ni dharura.