Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya kura ya veto yadhibitiwe

Matumizi ya kura ya veto yadhibitiwe

New Zealand imetaka mataifa matano yenye ujumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yajidhibiti katika matumizi ya kura ya veto.Wito huo umetolewa siku ya Jumamosi na Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand Murray McCully wakati akihutubia mkutano wa 67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini New York Marekani.

Amesema kama inakumbukwa miaka ya mwanzo baada ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa New Zealand ilipinga matumizi ya kura hiyo yananayofanywa na mataifa hayo matano ambayo ni China, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Urusi ambayo yalisema kuwa kura hiyo ni lazima ili kulinda maslahi yao.

“Ombi langu kwa nchi hizo tano zenye ujumbe wa kudumu ni kwamba zizingatie kauli yao ya mwaka 1945. Na changamoto yangu kwao hii leo ni kwamba ziangalie mchakato ambao kwa pamoja zinaweza kukubaliana kudhibiti matumizi ya kura hiyo turufu kwenye masuala ambayo bila shaka yanalinda maslahi muhimu ya taifa na kwamba yakubali bila shinikizo kujiepusha kutumia kura hiyo katika mazingira yanayosababisha maafa makubwa.”

Akizungumzia masuala yanayohusu ukanda wa Pacific, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa New Zealand amesema uvuvi haramu na vitendo vingine hatarishi vinaleta madhara kwa visiwa vidogo katika bahari hiyo ambavyo tegemeo lao kubwa ni uvuvi.