Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yaelelezea kujitolea kwake kusuluhisha mzozo na Sudan Kusini kwa njia ya amani

Sudan yaelelezea kujitolea kwake kusuluhisha mzozo na Sudan Kusini kwa njia ya amani

Serikali ya Sudan imesema itaendelea kutafuta suluhu kwa mzozo kati yake na Sudan Kusini kwa njia ya amani. Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Ahmed Karti katika hotuba yake kwenye kikao cha 67 cha mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York. Waziri huyo ameelezea pia kujitolea kwa taifa lake kutekeleza maazimio ya mkataba uliosainiwa mapema wiki hii baina yake na jirani wake Sudan Kusini.

Bwana Karti ametoa wito kwa Sudan Kusini iache kuunga mkono makundi ya waasi ambayo yanapigana dhidi ya serikali ya Sudan. Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa pia kuyashinikiza makundi ya waasi kwenye jimbo la Darfur yaweke chini silaha na kurejelea mazungumzo ya amani.

Kama mawaziri wengine waliomtangulia kutoka bara la Afrika, waziri Karti ametoa wito mfumo wa Baraza la Usalama ufanyiwe marekebisho, ili baraza hilo liwe na uakilishi zaidi. Amesema pia Umoja wa Mataifa unafaa kuendeleza heshima kwa uhuru na mipaka ya nchi wanachama, na kulaani waranta ya kumkamata rais wa Sudan, Omar al Bashir ilotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.