Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bara la Afrika ni lazima liwe na uakilishi kwenye Baraza la Usalama, wasema mawaziri kwenye mkutano wa Baraza Kuu

Bara la Afrika ni lazima liwe na uakilishi kwenye Baraza la Usalama, wasema mawaziri kwenye mkutano wa Baraza Kuu

Mawaziri kutoka bara la Afrika wameuambia mkutano wa Baraza Kuu kwamba wanataka lipanuliwe Baraza la Usalama ili bara la Afrika lipate uakilishi wa kudumu kwenye baraza hilo. Wakizungumza kwenye mkutano huo siku ya Jumamosi, mawaziri hao pia wamesisitizia umuhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kuhakikisha amani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mourad Medelci, amesema kuwa mfumo wa Baraza la Usalama ni lazima ufanyiwe marekebisho ili kuhakikisha kuna demokrasia, na kupanuliwa ili mataifa yanayoendelea yapate uakilishi, hususan bara la Afrika, ambako ustaarabu ulianza.

Naye waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritania, Ould Baba Hamadi, amesema nchi yake inaunga mkono mapendekezo ya kulifanyia marekebisho Baraza la Usalama, ili kuwepo kiti cha kudumu kwa bara la Afrika na mataifa ya Kiarabu. Akitaja matatizo yanayozikumba nchi zinazoendelea kama vile ukosefu wa ajira, mfumko wa bei ya chakula, ametoa wito kwa mataifa yaloendelea yatekeleza ahadi yalizoweka.