Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iceland kusaidia nishati asilia Afrika Mashariki

Iceland kusaidia nishati asilia Afrika Mashariki

Serikali ya Iceland imesema inanzisha programu ya kuzalisha nishati asilia na salama itokanayo na joto la ardhini kwa manufaa ya mamilioni ya wakazi barani Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iceland , Össur Skarphéðinsson, akihutubia mkutano wa 67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York , Marekani siku ya jumamosi, amesema nchi yake itashirikiana na Benki ya Dunia kusaidia mataifa 13 ya Afrika Mashariki kuzalisha nishati hiyo asilia.

(TAFSIRI YA OSSUR SKARPHEDINSSON)

Inaweza kuonekana kuwa jambo gumu lakini sisi Iceland tunapoamua kutumia utaalamu wetu wa kuzalisha nishati kwa kutumia joto la ardhini tunakuwa pia tumesaidia kulinda mazingira ya majirani zetu wa Arctic . Barafu ya Arctic inayeyuka kwa kasi kubwa kuliko ilivyotarajiwa.”

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Iceland pia amezungumzia matarajio ya kufungua baadhi ya maeneo ya Arctic ili yatumike kwa usafirishaji au kuzalisha gesi na mafuta.

Hata hivyo ameonya uwezekano wa mpango huo kuhatarisha mfumoanuai na maisha ya wakazi wa eneo hilo licha ya kwamba unaweza kuwa na manufaa ya kibiashara.