Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathiriwa wa ubakaji wa kuchochewa kisiasa Guinea-Conakry bado hawajapa haki: UM

Waathiriwa wa ubakaji wa kuchochewa kisiasa Guinea-Conakry bado hawajapa haki: UM

Kuna haja ya dharura ya kuwasaidia manusura wa wa machafuko yalofanyika Guinea-Conakry na kuwachukulia hatua za kisheria waliotekeleza ubakaji na uhalifu mwingine. Hayo ni kwa mujibu wa Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu dhuluma za ngono katika vita, Zainab Bangura, ambaye ametoa wito uchunguzi ufanywe na wahusika wote wawajibike ipasavyo.

Bi Bangura amesema kuwa ni muhimu pia waathirika wa uhalifu huo, na mashahidi wote na familia zao kulindwa kikamilifu, na nafasi yoyote isipotezwe kuhakikisha usalama wao wakati uchunguzi ukifanywa. Ameongeza kuwa watu wanaojulikana kuwa walitekeleza uhalifu huu wa ngono wasishikilie nafasi za uongozi, na kwamba kukabiliana na uhalifu huo ni muhimu katika kuendeleza maridhiano, imani kwa mfumo wa haki na amani ya kudumu.

Miaka mitatu iliyopita, uhalifu uliotekelezwa na vikosi vya serikali nchini Guinea-Conakry viliushtua ulimwengu, wakati wanawake walilengwa makusudi, na kubakwa hadharani. Vitendo hivyo vilionyesha sio tu kwamba ubakaji unatumiwa kama silaha ya vita, bali pia unatumiwa kufedhehesha, kunyamazisha, kutisha na kuadhibu waathiriwa.

Bi Bangura amesema Umoja wa Mataifa umejitolea kusaidia juhudi za serikali za kuhakikisha kuna haki na kwamba vitendo hivi havitarudiwa tena.