Vijana wanafaa kuwa nguzo katika maendeleo ya Somalia: UNDP

28 Septemba 2012

Huku zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya watu Somalia ikiwa ni vijana wenye umri chini ya miaka 30, kuwapa uwezo vijana itakuwa muhimu kwa ajili ya siku za baadaye za nchi hiyo, limesema Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP.

Hayo ni katika ripoti ya shirika hilo ya kwanza kwa zaidi ya mwongo mmoja, ambayo imezinduliwa siku ya Ijumaa. Ripoti hiyo inasema vijana wengi wanaamini kuwa wana haki ya kupata elimu na ajira nzuri, lakini wanavunjwa moyo kwa ukosefu wa nafasi za kupata vitu hivi.

Kwa sababu hiyo, shirika la UNDP linapendekeza kuwepo mabadiliko ya haraka ya kisera na mitazamo, ili vijana wapewe uwezo na kuwekwa kwenye nguzo ya kati ya mipango ya maendeleo. Ripoti hiyo inatoa wito ziundwe sera za kitaifa za vijana, pamoja na nafasi zaidi za kazi na misaada kwa mashirika ya vijana na miradi inayoanzishwa na vijana.

Ripoti hiyo pia ina mkataba wa vijana, ambao umeundwa na wawakilishi kutoka kote nchini Somalia na walioko ng’ambo, ambao utakuwa mwongozo wa kanuni za serikali, mashirika ya kutoa misaada na mashirika ya umma.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter