Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yalitaka bara la Afrika kuungana katika kudai uanachama wa Baraza la Usalama la UM

Tanzania yalitaka bara la Afrika kuungana katika kudai uanachama wa Baraza la Usalama la UM

Tanzania imetoa wito kwa bara la Afrika kuungana kuhusu suala la uakilishi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.  Katika hotuba yake kwa kikao cha 67 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa, Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania, Bernard Kamillius Membe, amesema kuwa bara la Afrika ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa, lakini pekee lisilo na uakilishi wa kudumu kwenye Baraza la Usalama.

Amesema hali hii pia inapuuza jambo lililo dhahiri kuwa, majadiliano mengi kwenye Baraza la Usalama yanalihusu bara la Afrika. Amesema Afrika inapaswa kuwa na viti viwili vya kudumu kwenye Baraza hilo, na kuyataka mataifa ya Afrika kuendeleza kasi ya kutaka hilo litimie.

Baraza la Usalama lina jukumu la kuhakikisha amani na usalama wa kimataifa, na wanachama wake wa kudumu ni Uchina, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani, na wote wana uwezo wa kukataa azimio lisipitishwe.

Bwana Membe pia amesema ulimwengu unafaa kuwa na desturi ya kutafuta suluhu la mizozo kwa njia ya amani. Akizungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa baada ya hotuba yake, amesema kuwa kuzuia mizozo ndio njia bora zaidi ya kukabiliana nayo.