Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugaidi wa kutumia silaha za nyuklia ni tishio kubwa zaidi: Rais wa Baraza Kuu

Ugaidi wa kutumia silaha za nyuklia ni tishio kubwa zaidi: Rais wa Baraza Kuu

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, amesema kuwa hakuna wazo linalotisha kama silaha za nyuklia kuwa mikononi mwa magaidi. Akihutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu kukabiliana na ugaidi wa kutumia silaha za nyuklia, Bwana Jeremic amerejelea ujumbe wake wakati wa kufungua mjadala wa Baraza Kuu, aliposema kwamba vita dhidi ya aina zote za ugaidi ni lazima liendelee kuwa jambo la kipaumbele.

Amesema ugaidi unahatarisha kuwepo kwa amani ya kudumu duniani, na kwamba juhudi zote zinapaswa kufanywa ili kuushinda. Ameongeza kwamba kama rais wa Baraza Kuu, atashirikiana na mataifa wanachama kuhusu jinsi watunga sera wa Umoja wa Mataifa wanaweza kuchangia utekelezaji wa mikakati ya kimataifa ilowekwa tayari ya kukabiliana na ugaidi.

Bwana Jeremic amesema anaamini kuwa hatua za pamoja zinafaa kuchukuliwa na mataifa wanachama ili kukamilisha mswada wa mkataba wa kina kuhusu ugaidi wa kimataifa, chini ya azimio nambari 66 aya ya 105.

(SAUTI YA VU JEREMIC)