Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Mugabe ataka kuheshimiwa misingi ya uanzishwaji UM

Rais Mugabe ataka kuheshimiwa misingi ya uanzishwaji UM

Huku akiidhihirishia hadhara ya kimataifa namna nchi yake ilivyotayari kuendeleza mashirikiano na jumuiya za kimataifa, rais wa Zimbabawe Robert Mugabe ametoa mwito akitaka Umoja wa Mataifa kutotumika kama kivuli cha kuhalalisha maslahi ya baadhi ya dola, akitolea mfano yale yaliyojitokeza katika nchi za Libya na Iraq.

Rais Mugabe ambaye alikuwa akizungumza kwenye hadhara ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa ametaka chombo hicho cha kimataifa kuanzisha dira mpya ili kukaribisha mageuzi na mabadiliko kwa shabaha ya kutoa fursa sawa kwa nchi wanachama na amesisitiza kutokuwepo kwa baadhi ya dola zinazokiuka misingi ya Umoja wa Mataifa na kuanzisha duru zinazopalilia maslahi binafsi.

Akiweka msisitizo katika hilo, rais Mugabe aliwakumbusha wajumbe kuhusu mkataba wa uanzishwaji wa Umoja wa Mataifa ambao alisema unaeleza wazi namna ya utendaji wa chombo hicho.

Alisema mkataba huo unasema kuwa utendaji wa Umoja wa Mataifa ni kwa maslahi ya watu wote duniani na siyo kutoa upendeleo kwa mataifa fulani.