Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kukomesha majaribio ya silaha za nyuklia na kuzitokomeza silaha hizo:Ban

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kukomesha majaribio ya silaha za nyuklia na kuzitokomeza silaha hizo:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameuambia mkutano wa mawaziri wa ngazi ya juu kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya kukomesha kufanya majaribio ya silaha za nyuklia na kuzitokomeza silaha hizo.

Akiwahutubia mawaziri hao kutoka mataifa wanachama wa mkataba wa kupiga marufuku majaribio ya nyuklia, Bwana Ban amesema kuwa ikiwa majaribio ya silaha za nyuklia yatakoma, basi uundaji wa silaha hizo pia utakoma.

Amesema mataifa ambayo hadi sasa hayajatia saini mkataba huo yanashindwa kutekeleza wajibu wao kama wanachama wa jamii ya kimataifa. Ameyasifu mataifa yaliyounga mkono mkataba huo, na kusema kuwa yamefanya uchaguzi wa busara kwa kuchagua usalama badala ya vitisho, amani badala ya vita na ubora wa dunia nzima badala ya matakwa ya taifa binafsi. Amesema mataifa haya yameonyesha uongozi mzuri, na kuonyesha desturi nzuri ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia.