Hakuna suluhu ya kijeshi kwa mzozo wa DRC:Ban

27 Septemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa uhuru na mipaka ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo haviwezi kukiukwa, na ni lazima viheshimiwe na nchi zote jirani zake. Bwana Ban amesema hayo katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambao umefanyika leo mjini New York.

Katibu Mkuu amesema hakuwezi kuwepo suluhisho ya kijeshi kwa mzozo uliopo nchini Kongo, na ni lazima wadau wote waone kwamba suluhisho ya amani inapatikana, kupitia mazungumzo, uhusishwaji wa wote na kujenga imani katika kila jimbo.

Bwana Ban amesema wote wanaokiuka haki za binadam ni lazima wawajibike kisheria, huku akitaja kuwa hali ya usalama imezorota katika majimbo yote ya Kivu, na kwamba makundi yenye silaha yanatumia hali hii kama kisingizio cha kutenda uhalifu. Ameongeza kuwa ubakaji na dhuluma zingine za ngono vinaendelea kutumiwa kama silaha za vita, na kuifanya mashariki ya Kongo kuitwa eneo la hatari zaidi ulimwenguni kwa mwanamke.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter