Skip to main content

Rais Kabila ayalaani makundi ya waasi nchini mwake kwenye UM

Rais Kabila ayalaani makundi ya waasi nchini mwake kwenye UM

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Joseph Kabila, ameonya kuhusu mizozo ya kutaka kujitenga inayolikumba taifa la Mali, pamoja na uharamia, njaa, umaskini na magonjwa yanayolikumba bara la Afrika. Rais Kabila ambaye taifa lake lenyewe limekumbwa na migogoro, amesema hata wakati anapozungumza mjini New York, maelfu ya watoto, wanawake na wanaume katika jimbo la Kivu ya Kaskazini hawana amani na wanakabiliwa na hali duni ya kibinadam.

Takriban watu 390,000 wanaishi kama wakimbizi wa ndani, baada ya kulazimika kuhama makwao, huku wengine zaidi ya 60,000 wakiwa wamekimbilia nchi jirani za Rwanda na Uganda, tangu mapigano yalipoanza kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa M23 katika jimbo la Kivu ya Kaskazini.

Rais Kabila ameyalaani makundi hasimu yanayoendesha mzozo huo, ambao amesema unaongozwa na watu wasioona aibu kutokana na uwezo wao wa kusababisha maumivu, na msaada wanaopata kutoka nje. Amesema watoto wamenyimwa nafasi ya kwenda shule, na badala yake, wanalazimishwa kutumia silaha kuwaua wanadamu wenzao, wakiwemo ndugu zao.