Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zuma aliambia Baraza Kuu la UM, bara la Afrika limepiga hatua za maendeleo

Zuma aliambia Baraza Kuu la UM, bara la Afrika limepiga hatua za maendeleo

Rais wa Afrika ya Kusini Jacob Zuma akizungumza katika baraza kuu ametoa heko kwa watu Somalia kwa kuchagua barabara ya amani na demokrasia, na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuendelea kuisaidia Somalia. Amesema bara la Afrika linapiga hatua za maendeleo, na ulimwengu mzima unapaswa kulisaidia katika hatua hizi.

Kuhusu ushirikiano wa kimataifa, rais Zuma amezungumzia haja ya kufanya kazi bega kwa bega ili kuyafikia malengo ya milenia, na hasa kupunguza umaskini na vifo kutokana na magonjwa kama kifua kikuu, UKIMWI na malaria. Amesema, mataifa yaloendelea yanatakiwa kuendelea kuchangia kutekeleza kwa malengo ya maendeleo ya milenia, ili kulisaidia bara la Afrika kuyafikia pia.

Bwana Zuma pia amezungumzia masuala mengi mseto, yakiwemo ubaguzi wa rangi ambao amesema unafaa kulaaniwa na kupingwa kwa vyovyote vile. Ametoa wito kwa mataifa yote kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Durban kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, na kuendeleza desturi ya kutatua mizozo kwa njia ya amani. Amesema Umoja wa Mataifa ni lazima uhakikishe haki, na usawa katika kukabiliana na mizozo yote, bila kufanya upendeleo.