Ghasia hazina nafasi katika Umoja wa Mataifa: Rais Obama

25 Septemba 2012

Akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Jumanne, rais wa Marekani, Barrack Obama, amesema ghasia na kutovumiliana havina nafasi miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Rais Obama amesema kuwa Umoja wa Mataifa ulianzishwa kwenye misingi ya dhana kuwa watu wanaweza kusuluhisha mizozo waliyonayo kwa njia ya amani, kupitia diplomasia.

Amesema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya ubalozi wa Marekani nchini Libya, hayakuwa mashambulizi dhidi ya Marekani tu, bali pia dhidi ya misingi ya dhana hiyo ya pamoja ya Umoja wa Mataifa.

"Ikiwa tunasema kuwa tunalinda kanuni hizi, haitoshi kuweka walinzi zaidi kwenye ubalozi, au kutoa taarifa za kuelezea kusikitishwa na kusubiri mambo kutulia. Ni lazima tuzungumze kuhusu chanzo hasa cha mzozo huu, kwani sasa tunakabiliwa na kuchagua kati ya vitu vitakavyotugawanya, na matumaini yetu ya pamoja.

Rais Obama ameanza hotuba yake kwa kutoa ujumbe wa heshima kwa balozi wa Marekani, Chris Stevens, ambaye aliuawa katika shambulizi mjini Benghazi, mashariki mwa Libya. Amesema balozi huyo alikuwa ishara ya picha halisi ya uzuri wa Marekani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter