Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, amesema mkataba mkuu wa Umoja wa Mataifa uliundwa ili kila taifa mwanachama lifuate sheria sawa na kuandama kanuni sawa. Amesema kwa kufanya hivyo, Umoja wa Mataifa ulikuwa na mtazamo wa kuwepo mfumo wa kimataifa wenye shabaha ya kuhakikisha sio tu usawa wa haki kwa kila taifa, bali pia heshima sawa kwa wote.

Bwana Jeremic ameuambia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa maumbile ya ulimwengu wa sasa ni ya kipekee, kwani ni ya kutegemeana. Amesema kuwa ulimwengu sasa unakabiliwa na changamoto nyingi, ambazo zinahitaji kuzingatiwa kwa umakini zaidi.

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema sasa ndio wakati wa ulimwengu kushirikiana kwa karibu zaidi, na kwamba rasilmali zote zinafaa kuelekezwa katika kuhakikisha hili. Amesema kwa kufanya hivyo, ulimwengu utatoa ufahamu mpya wa kusudio la msingi la mkataba mkuu wa Umoja wa Mataifa. Amesema kila mataifa yanapohisi yana usalama wa kutosha, basi hapo hulegeza mitazamo yao na kutoa nafasi kwa kusuluhisha mizozo kwa njia ya amani.