Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mdororo wa uchumi wa kimataifa unaumiza zaidi nchi maskini:UNCTAD

Mdororo wa uchumi wa kimataifa unaumiza zaidi nchi maskini:UNCTAD

Mdororo wa fedha na uchumi wa kimataifa umerudisha nyuma ukuaji wa kiuchumi katika nchi maskini zaidi duniani na kuondoma matumaini kuwa nusu ya nchi 48 maskini zitaweza kuondoka katika daraja hiyo katika kipindi cha mwongo mmoja, kama ilivyotarajiwa katika mkutano wa mwaka jana kuhusu nchi maskini. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti mpya wa Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD.

Utafiti uliofanywa katika nchi za Zambia, Benin na Cambodia unaonyesha kuwa mdororo wa uchumi wa hivi karibuni ulidhoofisha uwezo wa mataifa mengi maskini kuhakikisha kuwa kuna ujira wa kutosha na uwezo wa kununua bidhaa muihimu.

Nchini Zambia kwa mfano, kushuka kwa uzalishaji katika sekta ya kuchimba migodi kulipunguza mapato ya bidhaa zinazouzwa nje, ambayo yalilazimu kusimamishwa kwa baadhi ya shughuli za uzalishaji. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapato ya serikali yalipungua kwa asilimia 22 kati ya mwaka 2009 na 2010 kwa sababu ya hali hii. Nako nchini Benin, idadi ya watu wanaoishi katika umaskini wa kupindukia, ilipanda kutoka 33.4 hadi 34.4 kati ya 2007 na 2009.