Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaishukuru serikali ya Ethiopia kwa kusaidia kusambaza misaada ya chakula Sudan Kusini

WFP yaishukuru serikali ya Ethiopia kwa kusaidia kusambaza misaada ya chakula Sudan Kusini

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, limeishukuru serikali ya Ethiopia kwa kusaidia katika kudondosha misaada ya chakula kwa njia ya ndege kwa wakimbizi walioko kwenye kambi za Sudan Kusini.

Zaidi ya tani elfu moja za nafaka zilidondoshwa kwenye kata ya Maban Sudan Kusini na ndege ambazo ziliruka kutoka Gambrella kati ya mwezi Agosti na Septemba 17. Kwa mujibu wa WFP, hii iliruhusu kuendelea kusambaza chakula kwa wakimbizi ambao wametoroka mapigano katika jimbo la Blue Nile la Sudan na kufauta usalama Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la WFP nchini Ethiopia, Abdou Dieng, operesheni hiyo ya kudondosha chakula ilikuwa muhimu kuwafikishia wakimbizi 100, 000 chakula kwa njia ya haraka. Operesheni za WFP nchini Ethiopia sio tu muhimu katika kusambaza msaada wa chakula ndani mwa Ethiopia, bali pia katika kusaidia kazi ya shirika hilo nchini Somalia na Sudan Kusini. Mvua nzito zimesababisha usambazaji wa chakula kwa malori kuwa mgumu, na hivyo msaada wa kudondosha chakula kwa njia ya ndege ni muhimu kwa wakati huu.