Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la Afya litapewa kipaumbele katika mkutano wa 67 wa Baraza Kuu:Ban

Suala la Afya litapewa kipaumbele katika mkutano wa 67 wa Baraza Kuu:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema suala la UKIMWI na afya ya kimataifa kwa jumla litakuwa la kipaumbele katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu, ambao utafika kilele chake wiki ijayo. Bwana Ban amesema mjadala mkuu wa mwaka huu utakuwa wa hamasa kubwa zaidi, kwani kipindi cha sasa duniani ni cha mpito na migogoro. Itarajiwa kuwa yapata viongozi wa serikali 105 au mawaziri wa ngazi za juu watashiriki mjadala wa mwaka huu.

Baadhi ya mambo yatakayoangaziwa ni pamoja na hali inayozidi kuzorota nchini Syria; suala la hali ya dharura katika eneo la Sahel, hatua zilizopigwa katika harakati za kisiasa Somalia, hali inayotia moyo Myanmar na Yemen, migogoro iliyopo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na uhusiano kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Suala la ugaidi wa nyuklia na kupiga marufuku kabisa majaribio ya silaha za nyuklia litazingatiwa pia, pamoja na suala uongozi wa kisheria, katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Mkutano huo wa 67 pia utafuatilia malengo ya maendeleo ya milenia.