Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakaribisha hakikisho la Kenya kupunguza athari za operesheni zake za kijeshi Somalia

UM wakaribisha hakikisho la Kenya kupunguza athari za operesheni zake za kijeshi Somalia

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadam nchini Somalia, Mark Bowden, amekaribisha hakikisho kutoka kwa serikali ya Kenya kuwa jeshi lake litafanya kila liwezavyo kupunguza athari za operesheni zake dhidi ya raia nchini Somalia.

Katika taarifa yake baada ya kukutana na waziri wa Ulinzi wa Kenya, Mohamed Yusuf Haji, Bwana Bowden amesema waziri huyo amemhakikishia kuwa vikosi vya Kenya vitasaidia kuhakikisha kuwa watu wote wanaohitaji msaada wa kibinadam wanafikiwa. Bwana Bowden amekutana na waziri huyo wa ulinzi pamoja na kamanda mkuu wa jeshi la Kenya, Julius Karangi, ili kujadili jinsi ya kuwalinda raia wakati wa operesheni za kijeshi zinazoendesha na vikosi vya Kenya nchini Somalia.

Kuongezeka kwa mapigano katika siku chache zilizopita karibu na mji wa Kismayo Somalia, kumewalazimu watu wengi kuhama makwao kutoka mji huo.

Ametoa wito kwa pande zote katika mapigano kufanya kila ziwezavyo kupunguza athari za mapigano kwa raia, na kuruhusu misaada ya kibinadam kuwafikia.