Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani mauwaji ya mwandishi Tanzania,wataka uchunguzi huru

UM walaani mauwaji ya mwandishi Tanzania,wataka uchunguzi huru

Umoja wa Mataifa umelaani vikali mauwaji ya mwandishi wa habari Davidi Mwongosi ambaye anadaiwa kulipuliwa na askari polisi wakati akiwa kazini katika Mkoani Iringa nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

Katika taarifa yake ya kulaani maiwaji hayo, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Irina Bokova ametaka kuanzishwa uchunguzi huru juu ya tukio hilo.

Amesema vyombo vya dola kama ilivyo taasisi nyingine zinapaswa kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na vinawajibika kutetea uhuru wa maoni.

Ameeleza kuwa jumuiya ya kimataifa inasubiri kuona serikali ya Tanzania ikianzisha uchunguzi huru na wa haki ili wahusika wa tukio hilo wanafikishwa mbele ya sheria.

Mwandishi huyo wa habari aliyekuwa akifanya kazi na kituo cha televisheni, alilipuliwa na bumu la machozi wakati akifuatilia mkutano wa chama kimoja cha siasa uliokuwa ukifanyika mkoani Iringa.