Haiti ipo kwenye njia, asema afisa wa Haki za Binadamu wa UM

17 Septemba 2012

Naibu Katibu Mkuu wa Haki za Binadamu, Ivan Simonovic, ameelezea dalili za kutia moyo nchini Haiti, lakini pia hatari zilizopo, wakati akihitimisha ziara yake ya siku nne nchini humo. Baadhi ya mambo ambayo ametaja kama ya kutia moyo, ni marekebisho ya hivi karibuni ya katiba, ambayo yatawapa wanawake asilimia 30 ya nafasi zote za umma na baraza la kikatiba, pamoja na uteuzi wa waziri wa masuala ya haki za binadam na vita dhidi ya umaskini ulokithiri na kushuka kwa idadi ya watu kambini kutoka milioni 1.5 hadi 370, 000.

Amesema taifa la Haiti lipo kwenye njia panda, na kwamba ikiwa hatua zinazofaa zitachukuliwa kuhusu masuala fulani muhimu, kuna matumaini ya maendeleo, ingawa pia kuna hatari ya kurudi nyuma. Amesema baraza jipya la uchaguzi ni lazima liwe lenye kuaminika na idadi kubwa ya watu katika uwanja wa kisiasa, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mikoani, mitaani na ubunge unafanyika bila kuchelewa, na kwa njia huru na haki, na bila kuwepo ghasia.

Bwana Simonovic amekuwa nchini Haiti kujadili changamoto zilizopo, kabla ya Umoja wa Mataifa kufanya mabadiliko katika wajibu wa ujumbe wake nchini humo, MINUSTAH, ambako amekutana na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali, na maafisa wa Umoja wa Mataifa, balozi mbali mbali na mashirika ya umma.