Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UM lahitimisha muhula wake wa 66

Baraza Kuu la UM lahitimisha muhula wake wa 66

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limehitimisha kipindi cha muhula wake wa 66, ambacho kilianza mwezi Septemba mwaka uliopita. Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon, amesema muhula wa 66 umekuwa mwaka wa matukio mengi, na kuongeza kuwa kimekuwa kipindi cha mpito, na chenye mitihani.

Bwana Ban amesema mkutano wa Rio+20 ulikuwa na matokeo dhabiti na ya kutia moyo, yakiwemo uzinduzi wa malengo ya maendeleo endelevu na mikakati mingine ambayo italeta mabadiliko.

Amesema Baraza Kuu limekuwa ukumbi muhimu kwa ajili ya mazungumzo muhimu kuhusu kutokomeza umaskini na kuwapa wanyonge afueni. Ametaja kuwa Baraza la 66 lilifanya mkutano muhimu kuhusu usalama wa nyuklia, pamoja na mkutano wa kwanza kabisa wa ngazi ya juu kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ambayo yanaongoza kama chanzo cha vifo kote duniani.