Huenda tabaka la ozoni likarejea hali yake ya kawaida miongo mitano inayokuja:Ban

17 Septemba 2012

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amepongeza juhudi za jamii ya kimataifa za kuilinda anga akiongeza kuwa wakati asilimia 98 ya gesi zinazochangia kuharibika kwa tabaka la ozoni zikiwa zimeondolewa sasa tabaka hilo liko kwenye mkondo wa kurejea tena kwenye hali yake ya kawaida miongo mitano inayokuja.

Akiongea wakati wa siku ya kimataifa ya kulinda tabaka la ozoni inayoadhimishwa kila tarehe 16 mwezi wa Septemba Ban alizishauri serikali na washirika wote kujitolea kukabilina na changamoto za kimazingira na kimaendeleo za nyakati hizi. Siku hiyo inaadhimisha mwaka wa 1987 wakati kulipotiwa sahihi makubaliano ya Montreal kuhusu kupunguza vitu vinayotajwa kuchangia kuharibika kwa tabaka la Ozoni.