Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay asikitishwa na kuenea ghasia kufuatia filamu chochezi ya kuudhi

Pillay asikitishwa na kuenea ghasia kufuatia filamu chochezi ya kuudhi

Kamishna Mkuu wa haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na kidini kufanya vyovyote wawezavyo kurejesha utulivu, kufuatia filamu chochezi na yenye kudhihaki Uislamu, ambayo imesababisha maandamano katika takriban nchi 15 duniani. Amelaani mauaji ya wanadiplomasia wa Marekani na wafanyakazi wa Libya kwenye ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, na ghasia ambazo zimefanyika huko na kwingineko.

Amesema filamu hiyo ilikuwa yenye nia mbaya nay a uchochezi, na inatoa picha potovu kuhusu Waislamu. Pillay amesema anaelewa ni kwa nini watu wanataka kuandamana kuipinga, na ni haki yao kufanya hivyo kwa njia ya amani, lakini amelaani vikali mauaji ya Benghazi na ghasia na uharibifu kwa ajili ya filamu hiyo. Amekaribisha hatua ya serikali ya Libya ya kuahidi kuwafikisha walotekeleza mauaji hayo mbele ya sheria.

Akitaja kuwa filamu hiyo ni mojawepo ya vitendo vya kukusudia kuziudhi dini fulani na wafuasi wake, na ambavyo vimesababisha ghasia na mauaji mbeleni, Pillay amesema wakati mwingine ni vyema kutovijali vitendo kama hivyo vya maudhi. Amesema tofauti si kati ya Waislamu na watu wasio Waislamu, bali idadi ndogo ya watu wenye hisia kali kwenye pande zote, na ambao kusudi lao ni kueneza uadui na migogoro.