Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waadhimisha siku ya kimataifa ya amani

Umoja wa Mataifa waadhimisha siku ya kimataifa ya amani

Hafla za kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani zimefanyika leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, na kwenye makao makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO mjini Paris.

Katika ujumbe wake kuhusu siku hiyo ambayo huadhimishwa kila Septemba 21, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa mateso na machungu wanayopitia watu sasa hivi duniani yanaonyesha jinsi gani desturi ya amani inavyohitajika kwa dharura.

Ameongeza kuwa, ili kukabiliana na vyanzo vya mizozo, tunatakiwa kuendeleza ufahamu wa utu wetu kwa pamoja. Akitoa mifano ya mapigano Syria na Mali, pamoja na mauaji ya Libya na maandamano mengine kufuatia filamu ya chuki na dhihaka kwa Mtume Mohammed, Bwana Ban amesema ni jambo la aibu watu kutumia uhuru wao wa kujieleza kuchochea chuki na umwagaji damu, au wengine kuonyesha hasira zao kwa kusababisha ghasia.

Ameongeza kuwa kunahitajika desturi inayoheshimu utu na uhai wa mwanadamu. Amesema la muhimu zaidi katika kuweka desturi ya amani, ni elimu, kwani kupitia elimu, watoto wanafundishwa kuepukana na chuki, na kuwa viongozi wenye hekima na huruma, na hivyo, kuweka msingi wa kudumu wa desturi ya amani.