Balozi Mahiga asema Somalia imepata mwanzo mpya kufuatia uchaguzi wa rais mpya

11 Septemba 2012

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia, Augustine Mahiga, amesema kuchaguliwa kwa rais mpya wa Somalia ni hatua kubwa kwenye barabara ya kufikia amani na ufanisi, na kuongeza kuwa hatua hiyo inatoa ujumbe wenye uzito mkubwa kwa bara zima la Afrika na ulimwengu mzima.

Mnamo siku ya Jumatatu Septemba 10, wabunge nchini Somalia walimchagua Hasan Sheikh Mahmoud kama rais mpya wa taifa hilo la Pembe ya Afrika, katika shughuli ambayo imetajwa kama tukio la kihistoria. Mpinzani wake wa karibu sana, Sheikh Sharif Ahmed, ambaye amekuwa rais wa serikali ya mpito, amekubali kushindwa katika uchaguzi huo, na kumpongeza rais mteule, Sheikh Mahmoud, ambaye amekuwa kiongozi wa upinzani.

Balozi Augustine Mahiga ambaye ameongoza na kuendesha harakati zote za mabadiliko hayo ya kisiasa, amesema licha ya kwamba bado kuna changamoto nyingi, uchaguzi wa rais ni hatua kubwa katika harakati za kisiasa za taifa la Somalia, na kuelezea furaha yake kwamba kumekuwa na ufanisi kama huu. Katika mahojiano na Radio ya Umoja wa Mataifa, Joshua Mmali amemuuliza kwanza Balozi Mahiga shughuli nzima imekwenda vipi?