Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wabunge wa Somalia wakutana kumchagua rais

Wabunge wa Somalia wakutana kumchagua rais

Wabunge nchini Somalia wamekutana kumchagua rais katika shughuli ambayo imetajwa kama tukio la kihistoria katika taifa hilo ambalo halijawa na serikali inayodhibiti mambo kwa miongo kadhaa.

Uchaguzi wa rais ndiyo hatua ya mwisho katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuweka serikali mpya kwa taifa hilo ambalo limevurugwa na vita. Jumla ya wagombea 25 wameshiriki katika uchaguzi huo.

Uchaguzi huo umeahirishwa mara kwa mara, na kushindwa kumchagua rais kwenye tarehe iliyowekwa awali ya kuhitimishwa kipindi cha serikali ya mpito, huku jamii ya kimataifa ikilishinikiza bunge hilo kumchagua rais haraka.

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia, Augustine Mahiga, amesema licha ya kwamba bado kuna changamoto nyingi, uchaguzi wa rais ni hatua kubwa katika harakati za kisiasa za taifa la Somalia. Amelisifu bunge la sasa kama lenye kuwa na idadi kubwa ya watu wenye kisomo cha juu, asilimia 60 kati yao wakiwa wamehitimu na shahada ya digrii.