Baraza Kuu laadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia

6 Septemba 2012

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao maalum cha kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia, ambayo kawaida huadhimishwa kila Agosti 29. Katika taarifa yake kuhusu siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kufanya majaribio ya silaha za nyuklia kunahatarisha afya ya mwanadamu na amani na utulivu kote duniani.

Bwana Ban amesema kuwa siku ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia inatoa nafasi muhimu ya kutoa wito kwa ulimwengu mzima kuzingatia hatari za silaha za nyuklia na athari zake, ambazo huwa ni za muda mrefu. Ameelezea pia hatari ya kuendelea kuwepo maelfu ya silaha za nyuklia.

Bwana Ban amesema kuwa tayari kuna mkataba wa kina kuhusu kupiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia, ambao unaungwa mkono na karibu ulimwengu mzima, lakini bado haujaanza kutekelezwa. Mkataba huo una lengo la kupiga marufuku aina zote za majaribio ya vilipuzi vya nyuklia kwa njia inayoweza kuhakikiwa. Amesema wakati ukisubiri kuidhinishwa na kuanza kutekelezwa mkataba huo, ni muhimu kuimarisha juhudi za kutokomeza kufanya majaribio ya silaha za nyuklia, na kuendeleza jitihada za kuwa na ulimwengu usiokuwa na silaha za nyuklia.

(CLIP YA BAN)