Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya uchumi wa Palestina kukua, matarajio ya siku zijazo yamezidi kudidimia:UNCTAD

Licha ya uchumi wa Palestina kukua, matarajio ya siku zijazo yamezidi kudidimia:UNCTAD

Matarajio ya maendeleo ya kiuchumi kuwepo kwa muda mrefu katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa yamezidi kudidimia, imeonya Kamati ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Biashara na Maendeleo, UNCTAD, katika ripoti yake ya kila mwaka ya misaada kwa Wapalestina.

Ripoti hiyo inasema kuwa ukuaji wa uchumi wa asilimia 9.9 ambao ulishuhudiwa katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa mwaka 2011 hautoi picha kamili ya mtazamo wa siku za baadaye, kwani ukuaji huo, hasa kwenye ukanda wa Gaza, unaonyesha tu shughuli za ukarabati ulofanyika baada ya uharibifu ulotekelezwa na operesheni ya vikosi vya Israel tokea Disemba 2008 hadi Januari 2009.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uchumi wa Ukanda wa Gaza ulikuwa kwa asilimia 23 mwaka 2011, huku ule wa Ukingo wa Magharibi ukikua kwa asilimia 5.2. Hata hivyo, ukuaji halisi wa jumla ulikuwa asilimia 10 chini ya kiwango cha mwaka 2005.