Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ya kimataifa lazima itimize ahadi zake katika kutekeleza wajibu wa kulinda:Ban

Jamii ya kimataifa lazima itimize ahadi zake katika kutekeleza wajibu wa kulinda:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa kuafikia wajibu wa kulinda katika mkutano wa Baraza Kuu mwaka 2005 ulikuwa ufanisi muhimu sio tu kwa Umoja wa Mataifa, bali pia kwa watu wote duniani.

Akiwasilisha ripoti yake ya nne ya kila mwaka kuhusu wajibu wa kulinda, Bwana Ban ametaja matukio manne makubwa ambayo yalitokea katika karne ya ishirini, na ambayo yalichagiza kuafikia kauli ya wajibu wa kulinda, yakiwemo mauaji ya kimbari ya Wayahudi ya Holocaust, Cambodia, Rwanda, na Srebrenica, pamoja na majanga mengine makubwa ambayo serikali binafsi zilishindwa kutimiza wajibu wao kuzuia, chini ya sheria ya kibinadamu ya kimataifa.

Amesema matukio haya yalihoji uwezo na kujitolea kwa jamii ya kimataifa kuwalinda watu kutokana na mauaji ya kimbari au kikabila, pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu na uchochezi wa matukio kama hayo. Amesema ingawa jamii ya kimataifa husema kuwa haitoruhusu haya kutendeka tena, kawaida ahadi hii haitekelezwi. Amesema ni muhimu mataifa wanachama na jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wao, na kuhakikisha kuwa raia, ambao kawaida ni wanyonge, hawateseki kwa sababu ya mizozo kuhusu mambo yalopita, akitoa mfano wa hali ilivyo sasa nchini Syria.