Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitopoteza nafasi yoyote katika kutafuta amani Syria: Brahimi

Sitopoteza nafasi yoyote katika kutafuta amani Syria: Brahimi

Mwakilishi wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za Kiarabu. Lakhdar Brahimi amesema kuwa hali nchini Syria imekuwa ikizorota kila uchao, na kwamba idadi ya vifo imefikia viwango vya ajabu, uharibifu umefikia viwango vya kuwa janga, na watu wanateseka mno.

Bwana Brahimi ambaye anamrithi Kofi Annan kama mwakilishi maalum, amesema kuwa atakutana na Katibu Mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarbabu, Nabil Al Araby hivi karibuni, na kuuzuru mji mkuu wa Syria, Damscus na nchi zote ambazo zipo katika nafasi ya kuchangia harakati za kisiasa nchini Syria ili zizae matunda, na kujenga taifa linaloenda sawa na matakwa ya watu wake, na yenye demokrasia.

Akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa katika wadhfa wake mpya, Bwana Brahimi amesema Syria ya siku zijazo itajengwa na WaSyria wenyewe, na wala si mtu mwingine, na kuongeza kuwa usaidizi wa jamii ya kimataifa unahitajika na kwa dharura.

Ameongeza kuwa hatopoteza nafasi ya kushiriki katika juhudi zozote za pamoja kwa ajili ya amani kwa watu wa Syria.