Zaidi ya Wasyria milioni 2.5 wanahitaji msaada:UM

31 Agosti 2012

Zaidi ya watu milioni 2.5 wanahitaji msaada wa kibinadamu nchini Syria, lakini ombi la misaada hiyo limefadhiliwa kwa asilimia 50 tu, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson. Bwana Eliasson amesema kuwa amesema anataraji kuwa juhudi za kuwafikia watu wanaohitaji msaada nchini Syria zitaungwa mkono, na kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuchagiza ufadhili zaidi kwa ajili ya operesheni zake. Jumla ya dola milioni 180 za kimarekani zinahitajika kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu nchini Syria.

“Tumepata asilimia 50 pekee ya ufadhili wa dola milioni 180 tulizoomba, na ni dhahiri kuwa tunahitaji rasilmali haraka sana ili tukabiliane na hali hii.”

Naye Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la UNHCR, Antonio Guterres, amesema kuwa ushirikiano wa kimataifa unahitajika, si tu katika kuchangia maombi ya ufadhili wa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Syria walioko nchi jirani, bali pia wale waliomo ndani ya Syria. Amesema jamii ya kimataifa inapaswa kusaidiana na nchi walipokimbilia wakimbizi hawa, zikiwemo Uturuki, Jordan, Lebanon na Iraq, ambazo zinaonyesha ukarimu mkubwa.

“Nadhani zinahitaji ukarimu kama huo kutoka kwa jamii ya kimataifa ili ziweze kukabiliana na changamoto hii. Kwa upande mwingine, nadhani ni muhimu kutambua kuwa, hakuna suluhu la kibinadamu kwa tatizo hili. Suluhu ni ya kisiasa, na ni Baraza la Usalama pekee ndilo linaloweza kufanya maamuzi ambayo yatawezesha kupata suluhu ya kisiasa haraka.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud