Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufanya majaribio ya silaha za nyuklia bado ni hatari kwa afya ya mwanadamu na amani duniani:Ban

Kufanya majaribio ya silaha za nyuklia bado ni hatari kwa afya ya mwanadamu na amani duniani:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kufanya majaribio ya silaha za nyuklia kunahatarisha afya ya mwanadamu na amani na utulivu kote duniani. Bwana Ban amesema hayo katika ujumbe wake kwenye siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia, ambayo huadhimishwa kila Agosti 29.

Bwana Ban amesema kuwa siku ya leo inatoa nafasi muhimu ya kutoa wito kwa ulmiwengu mzima kuzingatia hatari silaha za nyuklia na athari zake ambazo huwa ni za muda mrefu, pamoja na hatari ya kuendelea kuwepo maelfu ya silaha za nyuklia.

Bwana Ban amesema, wakati wa kuadhimisha siku hii, ni muhimu kuimarisha juhudi za kutokomeza kufanya majaribio ya silaha za nyuklia, na kuendeleza jitihada za kuwa na ulimwengu usiokuwa na silaha za nyuklia.

Katika kuadhimisha siku hii, taifa la Kazakhstan limeandaa kongamano la Astana-Semipalatinsk, lenye ujumbe: Kutoka kwa upigaji marufuku majaribio hadi kwa ulimwengu usokuwa na silaha za nyuklia, ambako mchakato mpya wa kupiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia, uitwao ATOM umezinduliwa.